William Kipchirchir Samoei arap Ruto (aliyezaliwa 21 Desemba 1966, Sambut, Kenya) ni mwanasiasa wa Kenya ambaye amehudumu kama rais wa tano wa Kenya tangu 13 Septemba 2022. Kabla ya kuwa rais, aliwahi kuwa naibu wa rais wa kwanza wa Kenya kutoka 2013 hadi 2022.
Maisha ya Ruto na elimu
Ruto alizaliwa katika kijiji cha Sambut huko Kamagut (Kaunti ya Uasin Gishu) kwa Daniel na Sarah Cheruiyot. Alilelewa katika familia ya kidini, na amekuwa mshiriki wa Kanisa la African Inland Church.
Ruto alianza masomo yake katika Shule ya Msingi ya Kamagut, kisha akahamishwa hadi Shule ya Msingi ya Kerotet (Kaunti ya Uasin Gishu) na akasomea Certificate of Primary Education (CPE) katika shule hiyo. Kisha aliendelea na Shule ya Sekondari ya Wareng (Kaunti ya Uasin Gishu) na baadaye Shule ya Upili ya Kapsabet (Kaunti ya Nandi), ambapo alipata elimu yake ya Ordinary Level and Advanced Level. Alijiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi, ambapo alifuzu na BSc. katika botania na zoolojia (1990). Baadaye aliendelea na masomo yake katika taasisi hiyo, na kupata M.S. (2011) na Ph.D (2018) katika masomo ya Plant Ecology.
Ruto ameoa Rachel Chebet. Kwanza waliishi Dagoretti, Nairobi ambapo walipata mtoto wao wa kwanza. Walifunga ndoa mwaka wa 1991 katika Kanisa la Africa Inland Church. Kwa sasa wana watoto sita. Ruto pia ana binti na Prisca Chemutai Bett.
Ruto ameeleza mara kwa mara jinsi alivyouza karanga na kuku kando ya barabara ili kupata pesa. Miaka mingi baadaye, alifanikiwa kufungua miradi mingi ya kibiashara, kama ya kilimo na hoteli.
Kuingia kwa Ruto kwenye siasa
Baada ya kuhitimu kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi mnamo 1990, Ruto aliajiriwa kama mwalimu wa muda katika eneo la North Rift nchini Kenya kuanzia 1990 hadi 1992, ambapo pia alikuwa kiongozi wa kwaya ya kanisa la Africa Inland Church (AIC).
Ruto alijihusisha na siasa mwaka wa 1992, alipokuwa mweka hazina wa kikundi cha kampeni cha Youth for KANU 1992 (YK’92) kilichokuwa kikishawishi kuchaguliwa tena kwa Rais Daniel Arap Moi wa chama cha Kenya African National Union (KANU).
Alichaguliwa kwa mara ya kwanza Bungeni mwaka wa 1997 kama mbunge wa Eldoret Kaskazini. Ruto alihudumu kama waziri msaidizi katika Afisi ya Rais kuanzia 1998 hadi 2002 alipopandishwa cheo na kuwa Waziri wa Masuala ya Ndani ya Nchi kufuatia kufutwa kazi kwa George Saitoti na Rais Moi baada ya kutofautiana kuhusu urithi wa mamlaka 2002. Moi alipomchagua Uhuru Kenyatta kuwa mgombeaji urais wa chama katika uchaguzi wa 2002, Ruto alichagua kusalia katika chama hicho na kuunga mkono azma ya Kenyatta ya kuwania urais.
Ruto alikuwa katibu mkuu wa KANU mwaka wa 2005. Mwaka huo serikali ilifanya kura ya maoni kuhusu katiba mpya. Ruto alipinga katiba hiyo na kuunda muungano kutoka vyama vingine vya kisiasa kama Orange Democratic Movement (ODM) ya Raila Odinga ili kufanya kampeni dhidi ya katiba mpya. Aliimarisha msingi wake wa wapiga kura katika Mkoa wa Bonde la Ufa na ODM ilishinda katika kura ya maoni na katiba haikupita.
Mnamo Januari 2006, Ruto alitangaza kwamba atawania urais katika uchaguzi mkuu ujao (2007). Kauli hii haikupokelewa vyema na KANU. Kwa hivyo, badala yake alitaka uteuzi wa Orange Democratic Movement (ODM), lakini akapoteza uteuzi wa ODM kwa Raila Odinga. Ruto alimuunga mkono Raila baada ya kushindwa. KANU chini ya uongozi wa Uhuru Kenyatta iliamua kumuunga mkono Kibaki, na alijiuzulu wadhifa wake kama katibu mkuu wa KANU tarehe 6 Oktoba 2007.
Uchaguzi wa urais wa Desemba 2007 ulimalizika kwa msukosuko. Tume ya uchaguzi ya Kenya ilimtangaza Kibaki kuwa mshindi, lakini Raila wa ODM akadai ni yeye aliyeshinda. Mwai Kibaki aliapishwa kama rais na kukawa na mzozo mkali wa kisiasa nchini Kenya. Baadaye Kibaki na Raila walikubali kuunda serikali ya kugawana madaraka. Katika Baraza la Mawaziri la muungano huo wa Kibaki na Raila, Ruto aliteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo. Ruto pia alikua Mbunge wa Eldoret Kaskazini kuanzia 2008 hadi 4 Machi 2013.
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ilifungua uchunguzi kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007-08. Ilitoa majina ya watu sita waliodhaniwa kuhusika zaidi na kuchochea ghasia, na Ruto na Kenyatta walikuwa miongoni mwa waliotajwa. Mnamo Januari 2012 Ruto alishtakiwa kwa kuhusika katika kuchochea ghasia baada ya uchaguzi, dhidi ya makabila ambayo Kibaki alipata kuungwa mkono sana.
Ruto kama naibu rais wa Kenya
Bila kukatishwa tamaa na mashtaka yake ya ICC, Ruto aliungana tena na Kenyatta, na hao wawili na vyama vyao walijiunga na muungano wa vyama vingi na kuunda Muungano wa Jubilee, walishiriki uchaguzi wa Machi 2013 dhidi ya Raila Odinga na wakaibuka washindi.
Katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 2017, Uhuru na Ruto tena walitangazwa washindi baada ya kupata asilimia 54 ya kura zote zilizopigwa. Hata hivyo, Mahakama ya Juu ya Kenya ilibatilisha uchaguzi huo, na uchaguzi mpya ulifanyika Oktoba 2017. Upinzani ulisusia uchaguzi mpya na Uhuru na Ruto walichaguliwa tena kwa 98% ya kura zote zilizopigwa.
Ruto kama rais wa Kenya
Ruto aliwania uchaguzi wa urais wa 2022 kwa tiketi ya UDA chini ya Muungano wa Kenya Kwanza. Mnamo Agosti 15, mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati alimtangaza Ruto kuwa Rais mteule wa Kenya baada ya kupata asilimia 50.49 ya kura dhidi ya asilimia 48.85 ya Raila Odinga.
Raila alipinga matokeo hayo katika Mahakama ya Juu. Hata hivyo, Mahakama ya Juu iliidhinisha ushindi wa Ruto.
Tarehe 13 Septemba 2022, Ruto alitawazwa kuwa rais wa Kenya katika uwanja wa kimataifa wa Moi, Kasarani katika hafla iliyoongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome, na kuhudhuriwa na zaidi ya marais 20 wa nchi mbalimbali.
One response to “Maisha ya William Ruto”