Ngeli zote za kiswahili na mifano

Ngeli ni nini?

Ngeli ni mfumo wa kisarufi katika lugha ya Kiswahili ambao hutumia viambishi awali ili kuonyesha jinsia, wingi, na hali ya nomino.

Ngeli za Kiswahili

Kuna ngeli ya:

  • A-WA
  • U-I
  • LI-YA
  • YA-YA
  • KI-VI
  • I-ZI
  • I-I
  • U-ZI
  • U-YA
  • U-U
  • KU-KU
  • PA/KU/MU

Ngeli ya A-Wa

Hii ni ngeli ya majina ya viumbe wenye uhai kama vile watu, wanyama, ndege, wadudu, miungu, Malaika. n.k

Majina mengi katika ngeli ya A-WA huanza kwasauti M- kwa umoja na sauti WA- kwa wingi. Hatahivyo baadhi ya majina huchukua miundo tofauti.

Mifano ya nomino katika ngeli ya A – WA:
  • Wanadamu: mtoto, ndugu, msamaria, daktari, kiongozi
  • Wanyama: ng’ombe, mbuzi, swara, nyati, nguchiro
  • Ndege: bata, kuku, njiwa, mwewe, kipanga
  • Viumbe wa majini: samaki, papa, pweza, nyangumi na mamba
  • Wadudu: mende, mbu, kipepeo, nondo na nzi
  • Matakatifu wa kiimani: Mungu, Yesu, Mtume Mohammed na Malaika Israfili
  • Viumbe wasababishao zahama: jinni, pepo, na shatani

  Mfano wa sentensi:

  • Petero «a»mejenga nyumba.
  • Petero na Yohana «wa»mejenga nyumba.

Ngeli ya U-I

Huwakilisha majina ya vitu visivyo hai. Huwa na majina ya mimea, sehemu za mwili, vifaa, matendo, maumbile, na kadhalika. Kiambishi {–u} katika umoja na {–i} katika wingi

 Mfano:

  • Miti / mimea: mwiba-miiba, mkoma-mikoma, mwembe-miembe, mchai-michai
  • Vifaa: mkebe-mikebe, mtambo-mitambo, msumari-misumari
  • Maeneo: mji-miji, mtaa-mitaa
  • Maumbile: mlima-milima, msitu-misitu
  • Vipindi: msimu-misimu, mwaka-miaka

Mfano katika sentensi

  • Mtihani «u»mefanyika.
  • Mitihani «i»mefanyika.
Miundo ya ngeli ya U-I
  • M- mi; mti – miti
  • Mw- mi; mwenendo – mienendo
  • Mu- mi; muwa – miwa
  • Mt-Mi; mtego- mitego

Ngeli ya LI-YA

Inahusisha nomino zinazoanza kwa “Ji” katika umoja na “Ma” katika wingi.

Baadhi ya nomino hazina kiambishi ngeli katika umoja lakini katika wingi huchukuwa kiambishi “Ma”.

Mifano:

  • Jino limeng’oka (Umoja) – Meno yameng’oka (Wingi)
  • Jicho limevimba (Umoja) – Macho yamevimba (Wingi)
  • Tunda limeoza (Umoja) – Matunda yameoza (Wingi)
Miundo ya ngeli ya LI-YA
  • JI-MA: jiwe-mawe, jina-majina
  • JI-ME: jiko-meko, jino-meno
  • kapa-MA: gari – magari, jembe –majembe, jani-majani, jitu –majitu
  • kapa-kapa: joto-joto, jua-jua, jasho-jasho

Ngeli ya KI-VI

Ngeli ya KI-VI inatumiwa kuashiria hasa viumbe visivyo na uhai.

Ngeli hii, huzijumuisha nomino zinazoambishwa kwa kiambishi “ki- “cha umoja na “vi-“cha wingi, katika upatanisho wa kisarufi.

Mfano:

  • Kijiko «ki»mepotea.
  • Vijiko «vi»mepotea.
Miundo ya nomino zinazoainishwa katika ngeli ya KI-VI
i. Muundo wa ki-vi

Muundo huu unahusu nomino zenye kiambishi {ki-} katika umoja na {vi-} katika wingi.

Hujumuisha nomino kutoka ngeli nyingine zinazogeuzwa zikawa katika hali ya udogo.

Mfano:

  • Kijito – Vijito
  • Kijibwa – Vijibwa
  • Kitoto – Vitoto
ii. Muundo wa ch – vy

Muundo huu huzihusisha nomino zenye mianzo ya {ch-} katika umoja na {vy-} katika wingi.

Mfano:

  • Chakula – Vyakula
  • Chombo – Vyombo
  • Choo – Vyoo
  • Chama – Vyama
  • Chungu – Vyungu
iii. Muundo wa ki –

Muundo huu unahusu nomino zinazochukua kiambishi {ki-} mwanzoni, ambacho hakibadiliki katika wingi.

Nomino hizi, huweza kuainishwa kwa kuzingatia migao mbalimbali.

Mfano:

Majina ya Lugha mbalimbali.

Kama vile;

  • Kiswahili
  • Kiingereza
  • Kiajemi
  • Kijerumani
  • Kihausa

Majina yanayowakilisha baadhi ya hali.

Kama vile;

  • Kiwewe
  • Kichefuchefu
  • Kinyaa
  • Kimya

Majina ya baadhi ya majira au misimu.

Kama vile;

  • Kipupwe
  • Kifuku
  • Kiangazi

Majina ya baadhi ya magonjwa.

Kama vile;

  • Kiharusi
  • Kisukari
  • Kipindupindu
  • Kifaduro
  • Kichocho

Majina ya baadhi ya michezo.

Kama vile

  • Kibe
  • Kibafute

Majina ya harufu.

Kama vile;

  • Kikwapa
  • Kimenomeno
  • Kidusi
  • Kibeberu

Baadhi ya tabia.

Kama vile;

  • Kiherehere
  • Kibedi
  • Kiburi n.k.
Muundo wa – vi

Nomino zenye muundo huu huchukua kiambishi {vi-} mwanzoni pasi na kudhihirisha umbo la kiambishi cha umoja.

Mfano:

  • Vita
  • Vigelegele
  • Vitimbi
  • Virusi
  • Vimulimuli
  • Vifijo

Ngeli ya I-ZI

Hutumiwa kwa majina yasiyobadilika kwa umoja wala kwa wingi lakini huchukua viambishi viwakilishi tofauti: I- (umoja) na ZI- (Wingi). Mengi yake huanza kwa sauti /u/, /ng/, /ny/, /mb/.

  Mfano:

  • Ndizi «i»meiva (Umoja) – Ndizi «zi»meiva (Wingi)
  • Nyumba inajengwa (Umoja) – Nyumba zinajengwa (Wingi)

Uchambuzi wa ngeli hii hufuata mtazamo wa aina mbili: Nomino na Vivumishi.

Nomino

Nomino zinazoanza na N- inayofuata konsonanti ch, d, g, j, z, y, hubaki zilivyo katika umoja na wingi.

Mifano:

  • Nchi imepambwa. – Nchi zimepambwa.
  • Ndizi imeiva. – Ndizi zimeiva.
  • Nguo imechanika. –  Nguo zimechanika.
  • Njia hii inapitika. – Njia hizi zinapitika.
  • Nyota inaonekana angani. – Nyota zinaonekana angani.

Nomino zinazoanza na mb -, mv – umoja na wingi

Mifano:

  • Mbuga inalindwa vizuri. – Mbuga zinalindwa vizuri.
  • Mbegu ilipandwa hapa. – Mbegu zilipandwa hapa.

Nomino zilizotoholewa kutoka lugha ngeni.

Mifano:

  • Barua inafika. – Barua zinafika.
  • Kalamu imepotea. – Kalamu zimepotea.
  • Taa imezima. – Taa zimezima.
  • Meza imeletwa. – Meza zimeletwa.
  • Redio itanunuliwa kesho. – Redio zitanunuliwa kesho.
  • Karatasi imechanika. – Karatasi zimechanika.
Vivumishi vya sifa

Katika ngeli hii:

Vivumishi vya sifa vinavyoanzia konsonanti ch, f, p, k, t havina viambishi katika umoja wala wingi.

Mifano:

  • Nguo chafu imefuliwa. – Nguo chafu zimefuliwa.
  • Taa fupi inawaka. – Taa fupi zinawaka.
  • Meza pana imevunjika. – Meza pana zimevunjika.
  • Ndizi kubwa imeiva. – Ndizi Kubwa zimeiva.
  • Ndizi tamu imeliwa. – Ndizi tamu zimeliwa.

Vivumishi vingine huanza na n- au m- umoja na wingi.

Mifano:

  • Njia ndogo i hapa. – Njia ndogo zi hapa.
  • Mbegu mbaya imepandwa kule. – Mbegu mbaya zimepandwa kule.

Ngeli ya U-ZI

Ngeli hii hutumia kiambishi awali U- kwa umoja na ZI- kwa wingi kuonyesha nomino za vitu visivyo na uhai.

Majina katika ngeli hii huhusisha vitu vyembamba  na virefu ,yenye  wingi wa ‘ny’ au ‘m’ au ‘nd’ ambayo yanatumia upatanisho wa kisarufi wa ‘u’.

Mifano ya majina katika ngeli hii

1) ukucha – kucha.

2) Ulimi – ndimi

3) Ukuta – kuta

4) waya – nyaya

5) ufa- nyufa

6) ubawa – mbwawa

7) Wimbo – nyimbo

8)Wakati – nyakati

Mifano katika sentensi.

1) Ubawa wake umevunjika (umoja). Mbawa zake zimevunjika (wingi).

2) Ubavu wangu unaniuma (wingi). Mbavu  zetu zinaniuma (wingi).

3) Ukuta ule umebomoka (wingi). Kuta zile zimebomoka(wingi).

Miundo ya ngeli ya U-ZI

1. U-NY

Mifano

  • Uo-nyuo
  • Ufa-nyufa
  • Uga-nyuga
  • Uzi-nyuzi
  • Uta-nyuta

2. W-NY

Mifano

  • Wembe-nyembe
  • Waya-nyaya
  • Wayo-nyayo
  • Waraka-nyaraka
  • Wakati-nyakati
  • Wadhifa-nyadhifa

3. U**

Mifano

  • Uteo-teo
  • Ukoo-koo
  • Ukuta-kuta
  • Ufagio-fagio
  • Ufizi-fizi
  • Utaya-taya
  • Ushanga-shanga

Ngeli ya U-U

Huwa na nomino za dhahania na vitu visivyoweza kuhesabika.  Hazibadiliki kimaumbo.

Kiambishi {–u} katika umoja na {–u} katika wingi hutumika katika upatanisho wake wa kisarufi.

  Mfano:

  •  Ukaidi wake «u»limchongea.
  • Ukaidi wao «u»liwachongea.
Miundo ya nomino katika ngeli ya U-U
  • U-U:    Ujinga –Ujinga, Ulafi-ulafi, Ulaji –ulaji
  • WE-WE: Werevu-werevu
  • WI-WI:  wizi-wizi

Ngeli ya U-YA

Huwa na majina ya hali, matendo, na kadhalika. Kiambishi {–u} katika umoja na {–ya} katika wingi hutumika katika upatanisho wake wa kisarufi.

Mfano:

  •  Upishi wake  «u»mewavutia.
  • Mapishi yake  «ya»mewavutia.
Miundo ya ngeli ya U-YA.

U-MA: Ugonjwa – magonjwa, upana-mapana, uovu-maovu

Ngeli ya YA – YA

Nomino zinazoainishwa katika ngeli hii, huchukua kiambishi “ya- “cha upatanisho wa kisarufi katika hali zote.

Nomino hizi zinahusu vitu visivyohesabika kwa ubainifu na vilivyo katika wingi tu.

Mfano:

  • Mavune
  • Maumivu           
  • Manukato 
  • Maisha       
  • Mafuta 
  • Maarifa       
  • Mazingaombwe
  • Maasi
  • Mamlaka  
  • Makala n.k.

Mfano katika sentensi:

  • Maziwa yake «ya»meganda. (Umoja)
  • Maziwa yake «ya»meganda. (Wingi)
Miundo ya ngeli ya YA-YA

MA-MA: maji-maji, mauti – mauti, maziwa – mazingira.

Ngeli ya I-I

Huwa na nomino dhahania na vitu visivyoweza kuhesabika. Miundo ya nomino katika ngeli hii hazibadiliki katika umoja na wingi. Huchukua viambishi {i-i} katika umoja na wingi mtawalia.

 Mfano:

  • mihadarati-mihadarati
  • miwani-miwani
  • sukari -sukari
  • Chumvi «i»liyoletwa ni yake.
  • Chumvi «i»liyoletwa ni yao.

Ngeli ya KU-KU

Nomino zinazoundwa kutokana na vitenzi. Kiambishi {–ku} katika umoja na {–ku} katika wingi hutumika katika upatanisho wake wa kisarufi.

Mfano

  • Kuomba kwake kumemsaidia.
  • Kusoma kwake kumemsaidia
  • Kuinama huku kunachosha.

Ngeli ya PA-KU-MU

Hii ni ngeli ya mahali.

Huwa na nomino moja nayo ni ‘mahali’.

PA

Mahali karibu au panapodhihirika.

Mfano:

  • Mahali papendezavyo ni hapa.
  • Mahali hapa panapendeza.
KU

Mahali kusikodhihirika au mahali mbali.

Mfano:

  • Mahali kunakofaa ni huku.
  • Huku kwao kuna wezi.
MU

ndani ya

Mfano:

  • Mahali mnamofaa ni humu.
  • Shimoni mle mna takataka.

Ngeli za Kiswahili pdf

Hapa kuna ngeli za kiswahili pdf yeye unaenza download.

Related Posts