Lionel Messi ni mchezaji mashuhuri wa kandanda mzaliwa wa Argentina ambaye amepata kutambuliwa sana kwa ustadi wake wa kipekee na mchango wake katika soka. Alizaliwa Rosario, Argentina, Juni 24, 1987. Messi amekuwa akionyesha umahiri wake mara kwa mara katika soka, na hivyo kumwezesha kuvunja rekodi ya tuzo nane za Ballon d’Or. Ameshinda Ballon d’Or mwaka wa 2009, 2010, 2011, 2012, 2015, 2019, 2021 na 2023, ushindi huu ni ushahidi wa talanta yake isiyo na kifani na kujitolea kwake kwa soka.
Maisha ya utotoni
Lionel Messi, mzaliwa wa Rosario, Argentina, mwaka wa 1987, alionyesha kipaji mapema katika soka. Alilelewa katika mazingira ya soka, kwa hivyo alijipata akiwa amependa soka sana. Messi alijiunga na klabu ya Grandoli, ya huko Argentina, akiwa na umri wa miaka minne, baba yake ndiye aliyekuwa mkufunzi wa hiyo klub. Akiwa na miaka sita, alijiunga na Newell’s Old Boys, ambapo alionyesha talanta yake ya kipekee na kufunga karibu mabao 500 kwa timu ya vijana. Messi alikumbana na matatizo akiwa na umri wa miaka 10 alipogundulika kuwa na upungufu wa homoni za ukuaji, lakini licha ya matatizo ya kifedha, hatimaye alijiunga na akademi ya vijana ya Barcelona, La Masia, mwaka wa 2000.
Messi katika ngazi ya klabu
Barcelona
Licha ya matatizo yake, Messi alipata mafanikio katika timu ya vijana ya klabu ya Barcelona. Baada ya kumaliza matibabu ya homoni za ukuaji, alikua mchezaji muhimu wa Barcelona, akishinda mataji ya ligi na vikombe katika msimu wa 2002-03. Messi alipokea ofa kutoka kwa Arsenal lakini akachagua kubaki na Barcelona.
Safari yake ilianza 2004-05 alipokuwa mchezaji rasmi na mfungaji bora na mdogo katika Ligi ya Uhispania ya La Liga. Licha ya udogo wake, Messi alionyesha kipaji cha kipekee cha wepesi na udhibiti wa mpira. Mnamo 2005, alipata uraia wa Uhispania, na mwaka uliofuata, alichukua jukumu muhimu katika ushindi wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya wa Barcelona.
Ubora wa Messi uliendelea kuimarika, na kufikia 2008, alionekana kuwa mmoja wa wachezaji bora zaidi duniani. Mwaka wa 2009, aliisaidia FC Barcelona kutwaa mataji matatu ya kihistoria, na kushinda ubingwa wa La Liga, Copa del Rey, na Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya. Jambo hili lilimletea tuzo yake ya kwanza ya Ballon d’Or na Mchezaji Bora wa Dunia wa FIFA.
Umahiri wa Messi katika kupachika mabao uliendelea kung’ara, na kuvunja rekodi nyingi katika maisha yake Barcelona. Mnamo 2012, alivuka rekodi ya Gerd Müller ya kufunga mabao kwa msimu mmoja katika ligi kuu ya soka ya Ulaya, akiifungia Barcelona mabao 73. Pia alikua mfungaji bora wa muda wote wa Barcelona kwenye La Liga akiwa na umri wa miaka 24.
Aliiongoza Barcelona kutwaa mataji mengi ya La Liga na Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya, akiimarisha urithi wake kama mmoja wa wachezaji bora zaidi. Mnamo 2019, alipokea Ballon d’Or yake ya sita na akatangazwa Mchezaji Bora wa Wanaume na FIFA.
Licha ya matatizo ya kifedha, Messi aliendelea kujitolea kwa Barcelona kwa miaka mingi. Mnamo 2021, aliondoka katika klabu hiyo baada ya kuweka rekodi nyingi, ikiwa ni pamoja na kuwa mfungaji bora wa muda wote wa ligi ya La liga akiwa na mabao 474. Kuondoka kwa Messi kuliashiria mwisho wa enzi yake huko Barcelona.
PSG
Msimu wa kwanza wa Messi PSG ulikuwa mgumu, kwani alitatizika kuzoea klabu mpya na ligi. Alifunga mabao sita pekee katika Ligue 1, jumla ya mabao yake ya chini kabisa tangu 2005-06. Hata hivyo, alionyesha dalili za kuimarika katika msimu wake wa pili, na akatawazwa Mchezaji Bora wa Mwezi wa Ligue 1, Septemba 2022. Mnamo Februari 2023, alifunga bao lake la 700 akiwa na PSG, na alimaliza msimu akiwa na idadi kubwa zaidi ya pasi za mabao kwenye Ligue 1. Pia aliisaidia PSG kutwaa taji lao la 11 la Ligue 1 na la pili mfululizo tangu alijiunga nao.
Inter Miami
Lionel Messi alijiunga na klabu ya Inter Miami ya Marekani Julai 2023, akitia saini kandarasi ya miaka miwili na nusu. Alianza kuichezea klabu hiyo tarehe 21 Julai katika mechi ya Kombe la Ligi dhidi ya Cruz Azul, akifunga kwa mkwaju wa faulo katika dakika za lala salama kwa ushindi wa 2-1. Messi alicheza mechi yake ya kwanza ya MLS mnamo Agosti 26, akiingia kama mchezaji wa akiba katika dakika ya 60, akifunga bao la dakika za mwisho katika ushindi wa 2-0 ugenini dhidi ya New York Red Bulls. Kufuatia ushindi wake wa Kombe la Dunia akiwa na Argentina na kombe la Ligue 1 akiwa na PSG, Messi alitunukiwa tuzo ya Ballon d’Or, tarehe 30 Oktoba,2023, iliyoongeza rekodi yake ya tuzo hiyo hadi nane. Messi alimaliza msimu wake wa kwanza kwa Inter Miami akiwa na mabao 11 katika mechi 14.
Messi katika ngazi ya kimataifa
Safari ya Lionel Messi akiwa na Argentina imekuwa na mafanikio mengi na matukio ya kukumbukwa. Alichangia pakubwa katika ushindi wa Argentina katika Mashindano ya Dunia ya Vijana ya FIFA ya 2005 na ushindi wa medali ya dhahabu katika Michezo ya Olimpiki ya Beijing 2008, ambapo alifunga mabao mawili. Licha ya kukabiliwa na changamoto katika Kombe la Dunia la 2010 na 2014, alifanikiwa kupata tuzo ya Mpira wa Dhahabu mwaka wa 2010, licha ya kushindwa kwa Argentina na Ujerumani kwenye fainali. Azma ya Messi iliendelea, na akaiongoza Argentina kutinga fainali ya Copa América Centenario 2016, na kuvunja rekodi ya taifa ya ufungaji mabao.
Baada ya kustaafu kwa muda mfupi kufuatia kushindwa kwa fainali ya Copa 2016, Messi alirejea kuiongoza Argentina hadi nusu fainali ya 2019 ya Copa América na, hatimaye, ushindi katika michuano hiyo tarehe 10 Julai 2021. Kilele cha mafanikio yake ya kimataifa kilikuja katika Kombe la Dunia la 2022, ambapo Messi alifunga mabao mawili muhimu katika mchezo wa fainali dhidi ya Ufaransa, na kushinda Kombe la Dunia. Uchezaji wake bora ulimletea Mpira wa Dhahabu kwa mara ya pili katika historia ya Kombe la Dunia, na baadaye akashinda Ballon d’Or yake ya nane mnamo 2023, na kuimarisha hadhi yake kama mmoja wa wanasoka bora zaidi.