Mhariri Forum

Hadithi ya mwalimu …
 
Notifications
Clear all

Hadithi ya mwalimu Peter na mwanafunzi Zainab


Posts: 16
 oino
Topic starter
(@oino)
Eminent Member
Joined: 3 months ago

Kulikuwa na Mwalimu wa shule moja ya sekondari aliyeitwa Peter alikuwa amezoea kumchapa viboko mwanafunzi mmoja aliyeitwa Zainab kwa kosa la uchelewaji. Mwanafunzi huyu alikuwa akichelewa kipindi cha kwanza kila siku. Hivyo, siku ambazo mwalimu huyu alikuwa na kipindi cha kwanza, mwanafunzi huyu alikuwa anachapwa kwanza kabla ya kuingia darasani. Hali hii iliendelea kwa muda mrefu.

Wiki moja ilipita bila yule mwanafunzi kuonekana shuleni. Wiki iliyofuata yule mwanafunzi alifika shuleni mapema sana kabla ya mwanafunzi mwingine yeyote. Mwalimu yule alipomwona alifurahi sana. Alipoingia darasani alimwita yule mwanafunzi na kumsifia sana mbele ya darasa. “Zainab, simama. Darasa, Mpigieni makofi “Zainab” kwa sababu leo kawa wa kwanza kufika shuleni. Kumbe fimbo zile zimesaidia enhe” Wanafunzi walipiga makofi huku wengine wakimcheka huyo “Zainab”.

Baada ya wanafunzi kumcheka na kumfanyia dhihaka Zainab alimwomba mwalimu ampe nafasi aseme jambo. Mwalimu akamruhusu. Kwa sauti ya upole akasema, “Mwalimu, siku zote nilizokuwa nikichelewa kufika shule nilikuwa namuuguza mama yangu. Baba yangu alifariki kabla sijazaliwa. Nimelelewa na mama yangu tu. Simjui ndugu yeyote. Mama yangu alipokumbwa na maradhi alipelekwa hospitalini lakini maradhi yake hayakuonekana. Akaruhusiwa kurudi nyumbani akiwa na dawa za kutuliza maumivu tu. Kwa sababu hatuna pesa, hakuweza kupelekwa popote kwa vipimo zaidi.”

Zainab alifuta machozi yaliyoanza kutiririka mashavuni, akamtizama Mwalimu wake kisha akaendelea; “Hivyo kwa kipindi chote nilichokua namuuguza mama, nilitakiwa kufanya usafi wa nyumba, kuchota maji, kumsafisha mama yangu, kumwandalia chakula chake kabla ya kuja shuleni.” Zainab alinyamaza kidogo kisha akaendelea; “Lakini leo nimewahi kwa sababu mama yangu alifariki wiki iliyopita. Kwa hiyo kilichokuwa kinanichelewesha kimeondoka ndiyo maana leo nimewahi shuleni.”