Nomino ni nini?
Nomino ni aina ya neno inayotaja jina la mtu, mahali, kitu, au wazo.
Aina za nomino
- Nomino za pekee/maalumu /mahususi
- Nomino za kawaida
- Nomino dhahania
- Nomino za makundi/jamii
- Nomino za wingi/Fungamano
- Nomino za kitenzijina
- Nomino ambata
Nomino za pekee/ maalumu /mahususi
Nomino za pekee ni maneno yanayotaja majina mahususi ya watu, mahali, au vitu ambavyo vina sifa ya pekee. Nomino za pekee huanza kwa herufi kubwa.
Mifano ya nomino za pekee:
Watu: John, Mary, Barack Obama, Nelson Mandela
Maeneo: Dar es Salaam, Nairobi, London, New York
Vitu: Mwezi, Jua, Dunia, Bahari
Mifano yake katika sentensi
i) Mto Nzoia hufurika wakati wamasika.
ii) Paulo ameenda sokoni sasa hivi.
iii) Nairobi ndio mji mkuu wa Kenya.
iv) Ziwa Bogoria hupatikana katika eneo la Bonde la Ufa.
Nomino za kawaida
Hizi hutaja vitu kwa kawaida. Nomino hizi hurejelea dhana ,vitu au viumbe vinavyopatikana duniani.
Hizi ni nomino ambazo hazianzi kwa herufi kubwa ila tu zinapotumika mwanzoni mwa sentensi k.m.
i) Wanafunzi walishirikishwa kupanda miti mwaka huu.
ii) Wanafunzi watazuru ikulu ya raisi hiyo kesho.
iii) Wananchi hupaswa kutii sheria za nchi kila mara.
Mfano wa nomino za kawaida;
- Mtu
- Kitu
- Jino
- Redio
- Runinga
- Ukuta.
Nomino za dhahania
Nomino za dhahania ni maneno yanayotaja majina ya watu na vitu ambavyo ni vya kufikirika tu. Hapa chini ni mifano ya nomino dhahania.
Mifano ya nomino za dhahania
- Urembo
- Wema
- Upendo
- Uhai
- Ukora
- Umbeya
- Utawala
- Hekima
- Maarifa
- Busara
- Ujinga
- Ubaya
- Uchoyo
- Wazimu
- Ukeketaji
- Uzumbukuku
- Ucheshi
- Upuzi
- Wivu
- Chuki
Nomino za makundi/Jamii
Nomino za makundi au jamii ni majina yanayotajia mkusanyiko wa vitu, watu au wanyama.
Mifano ya nomino za makundi
- Kikosi cha askari
- Mkururo wa watoto
- Halaiki ya watu
- Mlolongo wa watu
- Kigaro cha wasingiziaji
- Kigaro cha wasengenyaji
- Kigaro cha wazushi
- Kambi ya wanajeshi
- Jopo la waandishi
Nomino za wingi/ Fungamano
Hizi huwa ni nomino ambazo hupatikana tu katika wingi na huwa haziwezi kuhesabika.
Kama vile; mate, mchanga, maji, mchele, sukari, chumvi, maziwa n.k.
Mfano katika sentensi
Waziri aliwahakikishia wanafunzi kuwa wakifanya vizuri katika mitihani ya kitaifa atawapa maziwa mengi.
Nyumba ilipoanza kuvuja maji yalijaa chumbani.
Nomino za kitenzi jina
Hizi ni nomino ambazo huundwa kutokana na vitenzi. Huundwa kwa kuambishwa. Kiambishi ‘ku’ kwenye mzizi wa kitenzi.
Kama vile; Kusoma, kula, kucheka, kucheza, kuimba, kulima, kukimbia n.k.
Mifano katika sentensi
Kusoma kwake kuliwafurahisKa wasikilizaji.
Mwanafunzi aliyependa kucheza darasani amefukunza ndakini.
Wanafunzi walikasirishwa na kucheka kwa bawabu.
Kulima kwa Bw.Bidii kuliwafurahisha watalii
Nomino ambata
Nomino amabata ni aina ya nomino inayoundwa kwa kuunganisha nomino mbili au zaidi kuwa neno moja. Nomino hizi mara nyingi hazina maana ya pamoja, lakini zinaunda maana mpya inapounganishwa.
Mifano ya nomino amabata:
- Askarikanzu – askari + kanzu
- Mwanamke – mwana + mke
- Mwananchi – mwana + nchi
- Mbwamwitu – mbwa + mwitu
- Pembetatu – pembe + tatu
- Batamzinga – bata + mzinga
- Simbamarara – simba + marara
- Mwanakamati – mwana + kamati