Vitenzi ni nini?
Vitenzi ni aina ya neno linaloeleza kitendo au hali inayofanywa na mtendaji.
Aina za vitenzi
- Vitenzi halisi
- Vitenzi vikuu
- Vitenzi visaidizi
- Vitenzi vishirikishi
- Vitenzi sambamba
Vitenzi halisi
Vitenzi hivi huwa na maana kamili katika sentensi, na hutumika peke yao katika sentensii bila kuandamana na vitenzi vingine.
Huwa na viambishi kabla na baada ya mzizi.
Mfano
Yeye anasoma. – ‘anasoma’ ni kitenzi halisi na kina kiambishi; a-kiambishi cha nafsi, na- wakati, som- mzizi, a- kiishio.
Kesho tutalima. – tu-kiambishi cha nafsi, ta- wakati, lim- mzizi, a- kiishio
Tunakimbia kwenda shule. n.k.
Vitenzi vikuu
Vitenzi vikuu hubeba maana kamili ya sentensi. Kitenzi kikuu lazima pawe na vitenzi kadhaa kwa sentensi ndipo kiwepo.
Mfano
Kifaru alikuwa akicheza ngoma asubuhi. – ‘alikuwa ‘ imetumika kama kitenzi kisaidizi. Kitenzi kikuu ni ‘akicheza’.
Sisi tulikuwa tunalima. – Tunalima ni kitenzi kikuu kwa sababu kinabeba maana kuu ya sentensi na pia kimeandamana na kitenzi kisaidizi ambacho ni “tulikuwa”
Aliponipigia, nilikuwa ninatazama filamu. – ‘ninatazama’ ni kitenzi kikuu, kimebeba maana kamili ya sentensi. ‘nilikuwa’ ni kitenzi kisaidizi.
Anapenda kutazama runinga. – ‘kutazama’ ni kitenzi kikuu, kimebeba maana kamili ya sentensi. ‘anapenda’ ni kitenzi kisaidizi.
Yazingatie yale niliyokwambia ili usije ukayasahau. – ‘ukayasahau’ ni kitenzi kikuu, kimebeba maana kamili ya sentensi. ‘usije’ ni kitenzi kisaidizi.
Vitenzi visaidizi
Huja kabla ya vitenzi vikuu au vitenzi halisi. Vitenzi visaidizi vinatoa msaada kwa vitenzi vikuu ili kuleta maana inayokusudiwa.
Hivi ni kama: kuwa, kuweza, kwenda, kupasa, kuwahi, kuja, kupenda, kwisha, kupata n.k.
Mifano wa sentensi
Sisi tulikuwa tunalima – Tulikuwa ni kitenzi kisaidizi: Kimekuja kabla ya kitenzi kikuu “tunalima” na pia kinasaidia katika kubeba maana ya sentensi.
Aliponipigia, nilikuwa ninatazama filamu. – kitenzi ‘nilikuwa’ husaidia kitenzi kikuu ‘ninatazama’.
Anapenda kutazama runinga. – kitenzi ‘anapenda’ kinakuja kabla na kinasaidia kitenzi kikuu ‘anatazama.
Yazingatie yale niliyokwambia ili usije ukayasahau.
Kifaru alikuwa akicheza ngoma asubuhi. – ‘alikuwa ‘ imetumika kama kitenzi kisaidizi. Kitenzi kikuu ni ‘akicheza’.
Vitenzi vishirikishi
Vinaitwa vitenzi vishirikishi kwa sababu hushirikisha kitu au mtu na hali au tabia fulani.
Vitenzi viki vimegawika katika aina mbili:
(a) vitenzi vishirikishi vikamilifu
(b) vitenzi vishirikishi vipungufu
Vitenzi vishirikishi vikamilifu
Huchukua viambishi vya ngeli, nafsi au vya wakati. Vitenzi hivi vinaweza kujisimamia peke yake au vinaweza kufuatiliwa na vitenzi vikuu.
Mifano
Babu angali na nguvu – ‘angali’ ni kitenzi kishirikishi kikamilifu maana kinashirikisha nomino “Babu” na hali ya “kuwa na nguvu” na pia kina viambishi ‘a-‘.
Chakula ndicho nguzo ya maisha. – ‘ndicho’ ni kitenzi kishirikishii kikamilifu maana kinashirikisha nomino ‘Chakula’.
Jibwa ndilo lilibweka asubuhi. – ‘ndilo’ ni kitenzi kishirikishii kikamilifu maana kinashirikisha nomino ‘Jibwa’.
Kanisani ndiko kuna sherehe yake. – ‘ndiko’ ni kitenzi kishirikishii kikamilifu maana kinashirikisha nomino ‘Kanisa’.
Vitenzi vishirikishi vipungufu
Havichukui viambishi
Huwa ni silabi moja tu mfano; zi, ki, li, vi, ni, si n.k
Mfano
Kalamu i mezani pako.
Nguo nzuri zi sandukuni.
Baba yangu ni Daktari.
Babu yu chumbani.
Zena ni mwerevu.
Jugo si mchezaji.
Vitenzi sambamba
Vitenzi sambamba hutokea katika mfululizo wa vitenzi visaidizi na vikuu.
Mfano
Yohana angekuwa akisoma angefaulu. – Hapa, ‘angekuwa akisoma angefaulu’ ni vitenzi sambamba.
Wawire alikuwa akiandika insha. – Vitenzi sambamba ni: ‘alikuwa akiandika’, ‘alikuwa’ ni kitenzi kisaidizi na ‘akiandika’ ni kitenzi kikuu.
Mwalimu anafundisha akiandika. – ‘anafundisha akiandika’ ni vitenzi sambamba.
Jemale alikuwa anazungumza akila ofisini. – ‘alikuwa anazungumza akila’ ni vitenzi sambamba.
Ogutu angali anachora vizuri. – ‘angali anachora’ ni vitenzi sambamba, ‘angali’ ni kitenzi kishirikishi kikamilifu na ‘anachora’ ni kitenzi kikuu.