Ngeli ya I-ZI
Katika ngeli ya I-ZI maneno hayabadiliki katika wingi. Majina mengi ya kukopwa kutoka lugha zingine hupatikana katika ngeli hii. Viambishi ngeli katika ngeli hii ni i katika umoja na zi katika wingi.
Hutumiwa kwa majina yasiyobadilika kwa umoja wala kwa wingi lakini huchukua viambishi viwakilishi tofauti: I- (umoja) na ZI- (Wingi). Mengi ya majina yake huanza kwa sauti /u/, /ng/, /ny/, /mb/.
Mfano:
- Ndizi «i»meiva (Umoja) – Ndizi «zi»meiva (Wingi)
- Nyumba inajengwa (Umoja) – Nyumba zinajengwa (Wingi)
Uchambuzi wa ngeli hii hufuata mtazamo wa aina mbili: Nomino na Vivumishi.
Nomino
Nomino zinazoanza na N- inayofuata konsonanti ch, d, g, j, z, y, hubaki zilivyo katika umoja na wingi.
Mifano:
- Nchi imepambwa. – Nchi zimepambwa.
- Ndizi imeiva. – Ndizi zimeiva.
- Nguo imechanika. – Nguo zimechanika.
- Njia hii inapitika. – Njia hizi zinapitika.
- Nyota inaonekana angani. – Nyota zinaonekana angani.
Nomino zinazoanza na mb -, mv – umoja na wingi
Mifano:
- Mbuga inalindwa vizuri. – Mbuga zinalindwa vizuri.
- Mbegu ilipandwa hapa. – Mbegu zilipandwa hapa.
Nomino zilizotoholewa kutoka lugha ngeni.
Mifano:
- Barua inafika. – Barua zinafika.
- Kalamu imepotea. – Kalamu zimepotea.
- Taa imezima. – Taa zimezima.
- Meza imeletwa. – Meza zimeletwa.
- Redio itanunuliwa kesho. – Redio zitanunuliwa kesho.
- Karatasi imechanika. – Karatasi zimechanika.
Vivumishi vya sifa
Katika ngeli hii:
Vivumishi vya sifa vinavyoanzia konsonanti ch, f, p, k, t havina viambishi katika umoja wala wingi.
Mifano:
- Nguo chafu imefuliwa. – Nguo chafu zimefuliwa.
- Taa fupi inawaka. – Taa fupi zinawaka.
- Meza pana imevunjika. – Meza pana zimevunjika.
- Ndizi kubwa imeiva. – Ndizi Kubwa zimeiva.
- Ndizi tamu imeliwa. – Ndizi tamu zimeliwa.
Vivumishi vingine huanza na n- au m- umoja na wingi.
Mifano ya sentensi katika ngeli ya i-zi
- Njia ndogo i hapa. – Njia ndogo zi hapa.
- Mbegu mbaya imepandwa kule. – Mbegu mbaya zimepandwa kule.
- Ndoo yangu ilipasuka. – Ndoo zangu zilipasuka.
- Nyumba ile ilibomolewa. – Nyumba zile zilibomolewa.
- Sahani imeoshwa. – Sahani zimeoshwa.
- Karatasi imeraruka. – Karatasi zimeraruka.
- Nyumba imejengwa. – Nyumba zimejengwa.
- Nguo imenunuliwa. – Wingi: Nguo zimenunuliwa.
- Penseli imepotea. – Penseli zimepotea.
- Pua inauma. – Pua zinauma.
- Shingo iliniuma sana nikiwa nyumbani. – Shingo zilituuma sana tukiwa nyumbani.