Maana ya kiambishi, aina za viambishi na mifano

Kiambishi ni nini?

Kiambishi ni silabi inayofungamanishwa na mzizi wa neno ili kuleta maana iliyokusudiwa. Viambishi haviwezi kusimama peke yao, bali lazima viunganishwe na mzizi wa neno. Kwa hivyo, kiambishi ni mofimu tegemezi inayoongeza maana fulani katika neno, kama vile ngeli, wakati, hali, mnyambuliko wa kitendo, n.k.

Aina za viambishi

Kuna aina mbili kuu za viambishi:

  • Viambishi awali
  • Viambishi tamati

Viambishi awali

Viambishi awali hutokea kabla ya mzizi wa neno. Kuna aina kadhaa za viambishi awali, kama vile:

  • Viambishi viwakilishi vya nafsi
  • Viambishi viwakilishi vya ngeli
  • Viambishi viwakilishi vya mahali
  • Viambishi viwakilishi vya wakati
  • Viambishi viwakilishi vya hali
Viambishi viwakilishi vya ngeli

Hizi ni silabi zinazowakilisha ngeli katika neno. Mfumo wa ngeli unaokubalika hutumia viambishi hivi kubainisha ngeli mbali mbali.

k.m:

a-me-som-a = kiambishi kiwakilishi cha ngeli ya A-WA (umoja)

zi-ta-pasuk-a = kiambishi kiwakilishi cha ngeli I-ZI wingi

ki-li-pote-a = kiambishi kiwakilishi cha ngeli ya KI-VI (umoja)

ya-na-angaz-iw-a = kiambishi kiwakilishi cha ngeli ya LI-YA (wingi)

Viambishi viwakilishi vya nafsi

Hivi ni viambishi ambavyo huonyesha nafsi katika neno. Kuna aina mbili za viambishi viwakilishi vya nafsi:

a) Viambishi Viwakilishi vya Nafsi ya Mtendaji/Mtenda

Hutumika kuonyesha aliyefanya kitendo katika neno. Kama viambishi vya Ngeli ya Mtendaji, viambishi hivi ndivyo vinavyotangulia viambishi vingine katika kitenzi.

Mifano wa nasfi umoja wingi

Nafsi ya kwanza NI TU: ni-na-andik-a, tu-li-shind-a

Nafsi ya pili U M: u-me-kasir-ik-a, m-na-pig-w-a

Nafsi ya tatu: A WA:  a-li-simam-a, wa-ta-p-ew-a

b) Viambishi Viwakilishi vya Nafsi ya Mtendewa/Mtendwa

Hutumika kuonyesha nafsi ya aliyeathirika na kitendo katika neno. Kama viambishi viwakilishi vya ngeli ya mtendewa, mara nyingi viambishi hivi huwekwa punde kabla ya shina la kitenzi.

Viambishi viwakilishi vya mtendewa ni sawa na viambishi viwakilishi vya mtendaji:

Mifano wa nafsi ya mtendewa:

Nafsi ya pili umoja KU: zi-me-ku-fik-i-a

Nafsi ya pili wingi M, MU, WA: ni-na-wa-tum-a

Nafis ya tatu umoja M: ni-ta-m-tambu-a

Viambishi viwakilishi vya Wakati/ Hali

Hivi ni viambishi ambavyo vinapowekwa kabla ya shina la kitenzi, vinatufahamisha wakati kitendo hicho kilipofanyika.

Mifano

LI: wakati uliopita kili-chom-ek-a

ME: wakati timilifu (uliopita muda mfupi) zi-me-anguk-a

NA: wakati uliopo tu-na-ku-subir-i

TA: wakati ujao wa-ta-ni-ju-lish-a

HU: wakati wa mazoea hu-som-e-a

A: wakati usiodhihirika a-tu-pend-a

KA: wakati usiodhihirika zi-ka-teket-e-a

PO: PO ya wakati a-li-po-wasil-i

KI: KI ya masharti ni-ki-zi-angali-a

Viambishi viwakilishi vya kukanusha wakati

Viambishi hivi hutumika kukanusha kitenzi katika sentensi kulingana na wakati au hali

Mifano

KU: wakati uliopita haku-ingi-a

JA: wakati timilifu (uliopita muda mfupi) si-ja-ku-uliz-i-a

-I: wakati uliopo na wa mazoea ha-som-i

TA: wakati ujao ha-ki-ta-maliz-ik-a

Tanbihi: Tunapokanusha wakati uliopo, wakati wa mazoea na wakati usiodhihirika, tunatumia kiambishi kiishio(I)

badala ya kutumia kiambishi tamati.

Kwa mfano: si-ku-ju-i, ha-pat-ik-an-i

Viambishi viwakilishi vya kukanusha nafsi

Tunapokanusha kitenzi, kiambishi cha kwanzwa hubadilika kulingana na nafsi.

Mifano

SI: nafsi ya kwanza si-ku-wa-on-a

HU: nafsi ya pili hu-ni-faham-u

HA: nafsi ya tatu ha-ta-chuku-a

Viambishi virejeshi vya ngeli

Hurejelea ngeli ya mtendewa au mtendwa na hutumika hasa katika vishazi tegemezi (vyenye o – rejeshi)

Mifano

wa-li-cho-nitum-i-a: kiambishi kirejeshi cha ngeli ya KI-VI

ni-ta-ka-ye-m-salim-i-a: kiambishi kirejeshi cha ngeli ya A-WA

u-li-ko-ji-fich-a: kiambishi kirejeshi cha ngeli ya mahali KU

tu-li-po-pa-safish-a: kiambishi kirejeshi cha ngeli ya mahali PO

Viambishi tama/tamati

Viambishi tama hutokea baada ya shina la kitenzi na hutumika kutuarifu kauli au myambuliko wa kitenzi hicho.

Viishio

Katika kauli ya kutenda, vitenzi vyenye asili ya Kibantu huishia kwa sauti “-a”. Kwa mfano: a-na-omb-a, tu-li-zo-andik-a

Tanbihi: Tunapokanusha vitenzi hivi vyenye asili ya Kibantu katika wakati uliopo na wakati wa mazoea kiishio “-a” hubadilika na kuwa “-i” Kwa mfano: Anapatikana- Hapatikani, Ninakujua-Sikujui.

Vitenzi vyenye asili ya kigeni huchukua viishio tofauti kama vile e, i na u katika kauli ya kutenda. Kwa mfano: ha-wa-ja-tu-jib-u, a-na-tu-subir-i, ni-me-ku-sameh-e Hata hivyo katika kauli nyinginezo (isipokuwa kauli ya kutenda) vitenzi hivi vya kigeni huchukua kiishio “a”. Kwa mfano harib-ik-a, tu-me-jib-iw-a

Viambishi viwakilishi vya kauli ya kitenzi

Hubadilika kulingana na mnyambuliko wa kitenzi.

Mfano

Kutendea “e, I”: omb-e-a, pig-i-a,

Kutendeana “ean, ian”: omb-ean-a, pig-ian-a,

Kutendwa “w”: som-w-a

Kutendewa “ew, iw”: omb-ew-a, pig-iw-a

Kutendeka “ek”: pend-ek-a

Kutendesha “esh, ez, ish, iz”: kom-esh-a, ing-iz-a

Kutendana “an”: finy-an-a.

Related Posts