Fasihi ni nini?
Fasihi ni sanaa inayotumia lugha au maneno katika sura mbalimbali kuwasilisha ujumbe unaomhusu binadamu.
Fasihi simulizi
Fasihi simulizi huwasilishwa kwa njia ya mdomo toka kizazi kimoja hadi kingine au masimulizi.
Sifa za fasihi simulizi
- Ni mali ya jamii nzima inayohusika.
- Ni kongwe kuliko fasihi andishi kwani imekuwepo tangu kuwepo kwa binadamu.
- Hadhira yake ni watu wote katika jamii; watoto, wazee, vipofu, viziwi na kadhalika.
- Hubadilika kulingana na mfumo wa jamii.
- Ina hadhira ya utendaji.
- Ina hadhira hai.
- Inaweza kubadilishwa papo kwa hapo ili kukidhi mahitaji ya hadhira.
- Huwasilishwa na fanani au masimulizi kwa njia ya masimulizi ya mdomo.
- Huhifadhiwa akilini na kusambazwa kwa njia ya masimulizi.
- Ina uhuru wa kutumia wahusika mbalimbali kama vile binadamu na viumbe vinginevyo.
- Ina tanzu nyingi kuliko fasihi andishi kama vile hadithi, semi, ngonjera, ushairi simulizi, maigizo.
Fasihi andishi
Fasihi andishi huwasilishwa kwa njia ya maandishi.
Sifa za fasihi andishi
- Ina tanzu chache kama vile riwaya, tamthilia, hadithi fupi na ushairi.
- Mara nyingi wahusika ni binadamu kwani inahusu binadamu na mazingira yake.
- Ni mali ya mwandishi aliyetunga.
- Huwasilishwa na mwandishi kwa njia ya maandishi.
- Huhifadhiwa kwa maandishi na kusambazwa kwa maandishi.
Tofauti kati ya fasihi simulizi na fasihi andishi
- Fasihi simulizi ina wahusika wa kila aina k.v binadamu, wanyama na ndege, mazimwi na majitu, miungu, mizimu, mashetani na vitu visivyo na uhai k.v. mawe na miti ilhali fasihi andishi ina wahusika binadamu kwa kiasi kikubwa.
- Fasihi simulizi ina tanzu nyingi kuliko fasihi andishi.
- Fasihi simulizi huwasilishwa kwa njia ya mdomo ilhali fasihi andishi huwasilishwa kwa njia ya maandishi.
- Fasihi simulizi huhifadhiwa akilini ilhali fasihi aandishi huhifadhiwa kwa maandishi.
- Fasihi simulizi ni mali ya jamii ilhali fasihi andishi ni mali ya mtu binafsi/mwandishi.
- Uwasilishaji wa fasihi simulizi huweza kuandamana na utendaji k.v matumizi ya ishara, nyimbo, makofi, kuimba ilhali fasihi andishi ni kwa maandishi tu.