Mistari na vifungu kuhusu hekima na maarifa kwenye biblia

Hapa utapata vifungu na aya za bibilia kuhusu hekima na maarifa. Mistari hizi zinasisitiza umuhimu wa kutafuta hekima, maarifa, busara na elimu, kukiri chanzo cha hekima kuwa ni Mungu, na faida zinazowaletea wale walio nazo.

Mistari na vifungu kuhusu hekima na maarifa kwenye biblia

Mithali 1:7 SRUV (SRUV: Swahili Revised Union Version)

Kumcha BWANA ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu.

Mithali 2:6 SRUV

Kwa kuwa BWANA huwapa watu hekima; Kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu

Mithali 3:13 SRUV

Heri mtu yule aonaye hekima, Na mtu yule apataye ufahamu.

Mithali 4:7 NEN (NEN: Neno: Bibilia Takatifu)

Hekima ni bora kuliko vitu vyote; kwa hiyo jipe hekima. Hata ikikugharimu vyote ulivyo navyo, pata ufahamu.

Mithali 9:10 SRUV

Kumcha BWANA ni mwanzo wa hekima; Na kumjua Mtakatifu ni ufahamu.

Mithali 10:14 SRUV

Watu wenye akili huweka akiba ya maarifa; Bali kinywa cha mpumbavu ni uangamivu ulio karibu.

Mithali 12:1 NEN

Yeyote apendaye kuadibishwa hupenda maarifa, bali yeye achukiaye kuonywa ni mpumbavu.

Mithali 15:33 SRUV

Kumcha BWANA ni maonyo ya hekima; Na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu.

Mithali 18:15 SRUV

Moyo wa mwenye busara hupata maarifa; Na sikio la mwenye hekima hutafuta maarifa.

Mithali 19:8 RSUVDC (RSUVDC: Biblia Kiswahili)

Apataye hekima hujipenda nafsi yake; Ashikaye ufahamu atapata mema.

Methali 24:13-14 BHN (BHN: Biblia Habari Njema)

Mwanangu, ule asali maana ni nzuri; sega la asali ni tamu mdomoni. Ndivyo ilivyo hekima nafsini mwako; ukiipata utakuwa na matazamio mema, wala tumaini lako halitakuwa la bure.

Mhubiri 7:12 BHN

Kulindwa na hekima ni kama kulindwa na fedha. Faida ya maarifa ni kwamba hekima hulinda maisha ya mtu aliye nayo.

Mhubiri 7:19 BHN

Hekima humfanya mwenye busara kuwa na nguvu zaidi kuliko watawala kumi mjini.

Mhubiri 8:1 BHN

Nani aliye kama mwenye hekima? Nani ajuaye hali halisi ya vitu? Hekima humletea mtu tabasamu, huubadilisha uso wake mwenye huzuni.

Danieli 2:23 BHN

Kwako, ee Mungu wa wazee wangu, natoa shukrani na kukusifu, maana umenipa hekima na nguvu, umetujulisha kile tulichokuomba, umetujulisha kile kisa cha mfalme.”

Wakolosai 2:2-3 BHN

Nafanya hivi kusudi mioyo yao ifarijiwe na kuvutwa pamoja katika upendo, ili wajazwe uthabiti mwingi uletwao na elimu ya kweli. Hapo wataijua siri ya Mungu ambayo ni Kristo mwenyewe. Ndani yake zimefichika hazina zote za hekima na elimu.

Yakobo 1:5 BHN

Lakini kama mmoja wenu ametindikiwa hekima, basi, anapaswa kumwomba Mungu ambaye atampatia; kwani Mungu huwapa wote kwa wingi na kwa ukarimu.

Yakobo 3:17 BHN

Lakini hekima itokayo juu mbinguni, kwanza ni safi; inapenda amani, upole na huwajali watu; imejaa huruma na huzaa matunda ya matendo mema; haina ubaguzi wala unafiki.

Zaburi 111:10 BHN

Kumcha Mwenyezi-Mungu ni msingi wa hekima; wote wanaozitii amri zake hujaliwa busara. Sifa zake zadumu milele.

Mithali 2:10-11

“Kwa maana hekima itaingia moyoni mwako, na ujuzi utapendeza nafsi yako. Busara itakulinda, na ufahamu utakulinda.”

Methali 16:16-23 BHN

16 Kupata hekima ni bora kuliko dhahabu; kupata akili ni chaguo bora kuliko fedha.

17 Njia ya wanyofu huepukana na uovu; anayechunga njia yake huhifadhi maisha yake.

18 Kiburi hutangulia maangamizi; majivuno hutangulia maanguko.

19 Afadhali kuwa mnyenyekevu na kuwa maskini, kuliko kugawana nyara na wenye kiburi.

20 Anayezingatia mafundisho atafanikiwa; heri mtu yule anayemtumainia Mwenyezi-Mungu.

21 Mwenye hekima moyoni huitwa mwenye akili; neno la kupendeza huwavutia watu.

22 Hekima ni chemchemi ya uhai kwake aliye nayo, bali upumbavu ni adhabu ya wapumbavu.

23 Moyo wa mwenye hekima humwezesha kusema kwa busara; huyafanya maneno yake yawe ya kuvutia.

Ayubu 12:13 SRUV

Hekima na amri zina yeye [Mungu]; Yeye anayo ushauri na fahamu.

Methali 26:17-28 BHN

Ajiingizaye katika ugomvi usiomhusu, ni kama mtu amshikaye masikio mbwa anayepita. Kama mwendawazimu achezeavyo mienge, au mishale ya kifo, ndivyo alivyo mtu ampotoshaye jirani, kisha aseme, “Nilikuwa natania tu!” Bila kuni, moto huzimika; bila mchochezi, ugomvi humalizika. Kama vile makaa au kuni huchochea moto, ndivyo mgomvi achocheavyo ugomvi. Maneno ya msengenyaji ni kama kitoweo; hushuka mpaka ndani kabisa tumboni. Kama rangi angavu iliyopakwa kigae, ndivyo yalivyo maneno matamu yenye nia mbaya. Mwenye chuki huficha chuki yake kwa maneno mazuri, lakini huwa ana hila moyoni mwake. Akiongea vizuri usimwamini, moyoni mwake mna chuki chungu nzima. Huenda akaficha chuki yake, lakini nia zake mbaya zitajulikana kwa wote. Amchimbiaye mwenzake shimo, hutumbukia mwenyewe; abingirishaye jiwe litamrudia mwenyewe. Asemaye uongo huwachukia hao anaowaumiza, naye abembelezaye huleta maangamizi.

Mithali 28:26 SRUV

Mwenye kujitumainia moyo wake ni mjinga; Bali yeye aendaye kwa busara ataokolewa.

Hosea 4:6 RSUVDC

Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi nami nitawasahau watoto wako.

1 Wakorintho 1:25 SRUV

Kwa sababu upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya wanadamu, na udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi ya wanadamu.

Mithali 8:10-11 BHN

10 Pokea mafundisho yangu, wala si fedha, Na maarifa kuliko dhahabu safi.

11 Maana hekima ni bora kuliko marijani; Wala vyote vinavyotamanika havilingani nayo.

Mithali 23:12 SRUV

Elekeza moyo wako kusikiliza mafundisho; Tega masikio yako kusikia maneno ya maarifa.

Isaya 11:2 BHN

Roho ya Mwenyezi-Mungu itakaa kwake, roho ya hekima na maarifa, roho ya shauri jema na nguvu, roho ya ujuzi na ya kumcha Mwenyezi-Mungu.

Zaburi 90:12 BHN

Utufundishe ufupi wa maisha yetu ili tuweze kuwa na hekima.

Related Posts